5 Kadhalika, Solomoni alijenga miji ifuatayo: Beth-horoni wa juu, na Beth-horoni wa chini, miji yenye ngome, kuta, malango na makomeo,
6 mji wa Baalathi, na miji yake yote ya ghala, magari yake ya kukokotwa na ya wapandafarasi wake, na chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, Lebanoni au kwingineko katika ufalme wake.
7 Watu wengine wote waliobaki miongoni mwa Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, yaani wote ambao hawakuwa Waisraeli,
8 pia wazawa wao ambao Waisraeli hawakuwaangamiza, Solomoni aliwafanyiza kazi za kulazimishwa, na hivi ndivyo wanavyofanya hata sasa.
9 Lakini kati ya watu wa Israeli, Solomoni hakumfanya mtu yeyote kuwa mtumwa kwa ajili ya kazi yake; wao walikuwa askari, makamanda wa maofisa wake, makamanda wa magari yake ya kukokotwa na wapandafarasi wake.
10 Ifuatayo ndiyo jumla ya maofisa wakuu wa mfalme Solomoni: Walikuwa 250, waliokuwa na mamlaka juu ya watu.
11 Solomoni alimhamisha binti Farao mfalme wa Misri, kutoka mji wa Daudi, akampeleka kwenye nyumba aliyomjengea. Alisema, “Mke wangu hataishi katika nyumba ya Daudi mfalme wa Israeli, kwa maana mahali pote ambapo sanduku la Mwenyezi-Mungu limekuwa, ni patakatifu.”