3 wakuu wa Waamori walimwambia bwana wao, Hanuni, “Je, unadhani kwamba Daudi kwa kukutumia watu wa kukufariji anamheshimu baba yako? Je, Daudi hakuwatuma watu hawa kwako ili kuuchunguza na kuupeleleza mji halafu wauteke?”
4 Basi, Hanuni aliwachukua wajumbe hao wa Daudi akamnyoa kila mmoja nusu ya ndevu zake, akayapasua mavazi yao katikati mpaka matakoni, kisha akawaacha waende zao.
5 Waliona aibu mno kurudi nyumbani. Daudi alipopashwa habari alituma watu kuwalaki kwani hao wajumbe waliona aibu sana. Naye mfalme aliwaambia, “Kaeni mjini Yeriko, hata mtakapoota ndevu, kisha mrudi nyumbani.”
6 Waamoni walipoona kuwa wamemchukiza Daudi, walikodi wanajeshi Waaramu 20,000 waendao kwa miguu, kutoka Beth-rehobu na Soba; wanajeshi 12,000, kutoka Tobu, na mfalme Maaka akiwa na wanajeshi 1,000.
7 Naye Daudi aliposikia habari hizo, alimtuma Yoabu kwenda na jeshi lote la mashujaa.
8 Waamoni walitoka na kujipanga tayari kwa vita kwenye lango la mji wa Raba, mji wao mkuu; nao Waaramu kutoka Soba na Rehobu na watu kutoka Tobu na Maaka walijipanga nyikani.
9 Yoabu alipoona kuwa vita ni vikali dhidi yake, mbele na nyuma, aliwateua baadhi ya wanajeshi Waisraeli hodari zaidi akawapanga kukabiliana na Waaramu.