16 Maana mfalme atanisikiliza na kuniokoa mikononi mwa mtu ambaye anataka kuniangamiza mimi pamoja na mwanangu kutoka urithi wa Mungu’.
17 Nami mjakazi wako nilifikiri kuwa, ‘Neno lake bwana wangu mfalme litanipa amani moyoni, kwani wewe bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kupambanua mema na mabaya.’ Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, awe pamoja nawe.”
18 Ndipo mfalme alipomjibu yule mwanamke, “Usinifiche jambo lolote nitakalokuuliza.” Yule mwanamke akasema, “Sema bwana wangu mfalme.”
19 Mfalme akamwuliza, “Je, Yoabu anahusika katika jambo hili?” Yule mwanamke akasema, “Kama uishivyo, bwana wangu mfalme, mtu hawezi kukwepa kulia au kushoto kuhusu jambo ulilosema bwana wangu mfalme. Yoabu yule mtumishi wako ndiye aliyenituma. Ni yeye aliyeniambia maneno yote haya niliyokuambia mimi mtumishi wako.
20 Yoabu alifanya hivyo ili kubadilisha mambo. Lakini, wewe bwana wangu, una hekima kama ya malaika wa Mungu hata unaweza kujua mambo yote yaliyoko duniani.”
21 Kisha, mfalme akamwambia Yoabu, “Sasa sikiliza, natoa kibali changu ili umrudishe nyumbani yule kijana Absalomu.”
22 Yoabu alianguka chini kifudifudi, akasujudu na kumtakia mfalme baraka, akasema, “Leo, mimi mtumishi wako, bwana wangu mfalme, ninajua kuwa nimepata kibali mbele yako, kwa kulikubali ombi langu.”