12 Lakini yule mtu akamwambia Yoabu, “Hata kama ningeuona uzito wa vipande 1,000 vya fedha mkononi mwangu, nisingeunyosha mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme. Maana, tulimsikia mfalme alipokuamuru wewe Abishai na Itai kwamba, kwa ajili yake, mumlinde kijana Absalomu.
13 Kwa upande mwingine, kama ningemtendea kwa hila (na hakuna lolote linalofichika kwa mfalme) wewe mwenyewe ungeniruka.”
14 Yoabu akamwambia, “Mimi sina wakati wa kupoteza pamoja nawe.” Hapo Yoabu akachukua mikuki midogo mitatu mkononi mwake, akaenda na kumchoma Absalomu moyoni, Absalomu akiwa bado hai kwenye tawi la mwaloni.
15 Kisha, vijana kumi waliombebea silaha Yoabu, wakaja kumzunguka Absalomu, wakampiga na kumwua.
16 Ndipo Yoabu akapiga tarumbeta na wanajeshi wote wakarudi kuwafuatia watu wa Israeli, kwani Yoabu aliwakataza.
17 Wakamchukua Absalomu wakamtupa kwenye shimo kubwa msituni na kurundika rundo kubwa sana la mawe. Watu wote wa Israeli wakakimbia, kila mmoja nyumbani kwake.
18 Absalomu, wakati wa uhai wake, alikuwa amejijengea na kujisimikia nguzo iliyoko kwenye Bonde la Mfalme, kwani alisema, “Mimi sina mtoto wa kiume wa kudumisha jina langu ili nikumbukwe.” Nguzo hiyo aliipa jina lake, na inaitwa “Nguzo ya Absalomu” mpaka leo.