2 Hivyo, Daudi alikwenda Hebroni, pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mjane wa Nabali, kutoka mji wa Karmeli.
3 Aliwachukua watu wake, kila mtu akiwa pamoja na jamaa yake; nao wakafanya makao yao katika miji iliyokuwa kandokando ya Hebroni.
4 Watu wa Yuda walimwendea Daudi huko Hebroni wakampaka mafuta awe mfalme wao.Daudi aliposikia kuwa watu wa Yabesh-gileadi ndio waliomzika Shauli,
5 aliwatuma watu huko Yabesh-gileadi na ujumbe: “Mwenyezi-Mungu na awabariki kwa maana mlionesha utii wenu kwa Shauli, bwana wenu, kwa kumzika.
6 Sasa, Mwenyezi-Mungu awafadhili na kuwa mwaminifu kwenu. Nami nitawatendea mema kutokana na jambo mlilolitenda.
7 Lakini muwe imara na mashujaa. Shauli, bwana wenu, amekufa, na watu wa Yuda wamenipaka mafuta niwe mfalme wao.”
8 Abneri mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Shauli alikuwa amemchukua Ishboshethi mwana wa Shauli na kumpeleka huko Mahanaimu.