12 Hivyo, Daudi akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu amemwimarisha awe mfalme wa Israeli, na kwamba ameukuza ufalme wake kwa ajili ya watu wake wa Israeli.
13 Daudi alijitwalia masuria na wake zaidi wa huko mjini Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni. Hao, wakamzalia watoto zaidi wa kiume na wa kike.
14 Yafuatayo ndiyo majina ya watoto wa kiume, wake zake waliomzalia huko Yerusalemu: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni,
15 Ibhari, Elishua, Nefegi, Yafia,
16 Elishama, Eliada na Elifeleti.
17 Wafilisti waliposikia kwamba Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wote walitoka kwenda kumtafuta, lakini yeye alipata habari, akaingia ndani ya ngome.
18 Wafilisti walifika na kujitawanya kwenye Bonde la Refaimu.