19 Hapo atageuka kurudi katika ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka vitani na huo ndio utakaokuwa mwisho wake.
20 “ ‘Huyu atafuatwa na mfalme mwingine ambaye atatuma mtozaushuru kupitia katika fahari ya ufalme wake. Mfalme huyo atauawa baada ya siku chache, lakini si kwa hasira wala vitani.
21 “ ‘Mfalme atakayefuata atakuwa baradhuli ambaye hana idhini ya kushika ufalme, naye atakuja bila taarifa na kunyakua ufalme kwa hila.
22 Majeshi pamoja na kuhani wa hekalu, atawafagilia mbali na kuwaua.
23 Kwa kufanya mapatano, atayahadaa mataifa mengine, na ataendelea kupata nguvu ingawa atatawala taifa dogo.
24 Bila taarifa atazivamia sehemu za mkoa zenye utajiri mwingi na kufanya mambo ambayo hayakufanywa hata na mmoja wa wazee wake waliomtangulia. Kisha, atawagawia wafuasi wake mateka, mali na vitu alivyoteka nyara vitani. Atafanya mipango ya kuzishambulia ngome, lakini kwa muda tu.
25 “ ‘Kwa ujasiri mwingi, ataunda jeshi kubwa ili kuushambulia ufalme wa kusini, naye mfalme wa kusini atajibu mashambulizi hayo kwa jeshi kubwa zaidi na lenye nguvu sana. Lakini, mfalme wa kusini hatafaulu kwani mipango ya hila itafanywa dhidi yake.