40 “ ‘Wakati wa mwisho mfalme wa kusini atamshambulia mfalme huyo wa kaskazini. Lakini mfalme wa kaskazini atajibu mashambulio hayo kwa nguvu kama kimbunga, akitumia magari ya farasi, wapandafarasi na meli nyingi. Atazivamia nchi nyingi na kupita katika nchi hizo kama mafuriko ya maji.
41 Ataivamia hata nchi ile tukufu na kuua maelfu ya watu. Lakini nchi za Edomu, Moabu na sehemu kubwa ya Amoni, zitaokoka kutoka mikononi mwake.
42 Wakati atakapozivamia nchi hizo, hata nchi ya Misri haitanusurika.
43 Atamiliki hazina za dhahabu, fedha na vito vyote vya thamani vya nchi ya Misri. Watu wa Libia na watu wa Kushi watafuata nyayo zake.
44 Lakini habari kutoka mashariki na kaskazini zitamtisha. Naye atatoka kwa hasira kubwa ili kukatilia mbali na kuangamiza wengi.
45 Zaidi ya hayo, atapiga mahema yake makubwa kati ya bahari na mlima mtukufu na mtakatifu. Lakini atakuwa amefikia kikomo chake, na hatakuwapo yeyote wa kumsaidia.