25 Kisha akauliza, “Lakini sasa mbona ninaona watu wanne wakitembeatembea humo motoni bila kufungwa na wala hawadhuriki, na mtu wa nne anaonekana kama mwana wa miungu?”
26 Basi, mfalme Nebukadneza akaukaribia mlango wa tanuri ya moto mkali, akaita, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Mkuu, tokeni mje hapa!” Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka motoni.
27 Maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa na washauri wa mfalme, wote wakakusanyika pamoja, wakaona ya kuwa ule moto haukuweza kuwaunguza hao watatu. Nywele zao hazikuungua, mavazi yao hayakuungua, wala hawakuwa na harufu yoyote ya moto.
28 Basi, mfalme Nebukadneza akasema, “Na asifiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego kwa kuwa alimtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake ambao wanamtegemea. Wao walikataa kutii amri yangu ya kifalme, wakaitoa mhanga miili yao badala ya kuabudu mungu mwingine, ila Mungu wao peke yake.
29 Kwa hiyo, naamuru kwamba watu wa kabila lolote, taifa lolote au lugha yoyote, watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, watangolewa viungo vyao kimojakimoja na nyumba zao zitabomolewa. Maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”
30 Basi, mfalme Nebukadneza akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika mkoa wa Babuloni.