5 Lakini nikaota ndoto iliyonitisha; nikiwa nimelala kitandani, mawazo na maono kichwani mwangu yaliniogopesha.
6 Hivyo, nikaamuru wenye hekima wote wa Babuloni waletwe mbele yangu ili wanieleze maana ya ndoto hiyo.
7 Ndipo waganga, walozi, Wakaldayo na wanajimu wakaletwa. Nikawasimulia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunieleza maana yake.
8 Baadaye, akaja Danieli, anayeitwa pia Belteshaza, jina la mungu wangu, ambaye roho ya miungu mitakatifu imo ndani yake. Nami nikamsimulia ndoto yangu, nikasema:
9 Ee Belteshaza, uliye mkuu wa waganga, nafahamu kuwa roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako, na kwamba hakuna fumbo lililo gumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu; niambie maana yake.
10 “Nilipokuwa nimelala, niliona maono haya: Niliona mti mrefu sana katikati ya dunia.
11 Mti uliendelea kukua, ukawa imara na kilele chake kikafika mbinguni. Uliweza kuonekana kutoka kila mahali duniani.