17 Kwa hiyo, ee Mungu, isikilize sala yangu na maombi yangu mimi mtumishi wako. Kwa hisani yako, uifadhili tena maskani yako iliyoharibiwa.
18 Tega sikio, ee Mungu wangu; angalia uone taabu tulizo nazo na jinsi unavyotaabika huo mji uitwao kwa jina lako. Tunakutolea maombi yetu si kwa sababu tumetenda haki, bali kwa sababu wewe una huruma nyingi.
19 Ee Mwenyezi-Mungu, utusikie; utusamehe ee Mwenyezi-Mungu. Ee Mwenyezi-Mungu, kwa hisani yako utusikie na kuchukua hatua, wala usikawie, ee Mungu wangu, kwa ajili ya mji huu na watu hawa wanaoitwa kwa jina lako!
20 “Basi, nilipokuwa nikiomba, nikiungama dhambi zangu na dhambi za watu wangu wa Israeli, pamoja na kumsihi Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya mlima wake mtakatifu,
21 yule mtu Gabrieli, ambaye nilikuwa nimemwona katika maono hapo awali, alishuka kwa haraka mpaka mahali nilipokuwa. Ilikuwa wakati wa kutoa sadaka ya jioni.
22 Basi, akaniambia, ‘Danieli, nimekuja kukupa hekima na uwezo wa kufahamu.
23 Ulipoanza kuomba, Mungu alitoa jibu, nami nimekuja kukueleza jibu hilo kwa kuwa unapendwa sana. Kwa hiyo, usikilize kwa makini jibu hilo na kuelewa maono hayo.