8 Aibu, ee Bwana, ni juu yetu, wafalme wetu, wakuu wetu na wazee wetu, kwa sababu tumekukosea.
9 Wewe, Bwana Mungu wetu, una huruma na msamaha, ingawa sisi tumekuasi.
10 Tulikataa kukusikiliza, ee Bwana, Mungu wetu; hatukuishi kulingana na sheria zako ulizotupa kwa njia ya watumishi wako manabii.
11 Waisraeli wote wameiasi sheria yako, wamekuacha wakakataa kukutii. Kwa sababu tumekukosea, tumemwagiwa laana na viapo vilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtumishi wako.
12 Umethibitisha yale uliyosema utatutenda sisi pamoja na watawala wetu kwa kuuadhibu mji wa Yerusalemu vikali zaidi ya mji mwingine wowote duniani.
13 Umetuadhibu kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, lakini mpaka sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, hatukuomba msamaha wako kwa kuziacha dhambi zetu na kutafakari uaminifu wako.
14 Kwa hiyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ulikuwa tayari kutuadhibu, na ukafanya hivyo, kwa kuwa daima unafanya yaliyo ya haki, nasi hatukukusikiliza.