3 Lakini Zerubabeli, Yeshua na viongozi wengine wa koo za Israeli wakawaambia, “Sisi hatuhitaji msaada wowote kutoka kwenu ili kuijenga nyumba ya Mungu wetu. Sisi wenyewe tutamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kama mfalme Koreshi wa Persia alivyotuamuru.”
4 Hapo, watu waliokuwa wanaishi mahali hapo wakaanza kuwavunja moyo na kuwatisha Wayahudi ili wasiendelee kama walivyokusudia.
5 Tena waliwahonga maofisa wa serikali ya Persia wawapinge Wayahudi. Waliendelea kufanya hivyo muda wote wa utawala wa Koreshi, mpaka wakati wa utawala wa Dario.
6 Mwanzoni mwa utawala wa mfalme Ahasuero, maadui wa watu waliokaa Yuda na Yerusalemu waliandika mashtaka dhidi yao.
7 Tena wakati wa utawala wa Artashasta, mfalme wa Persia, Bishlamu, Mithredathi, Tabeeli na rafiki zao, walimwandikia barua mfalme Artashasta. Barua hiyo iliandikwa kwa herufi za Kiaramu na kutafsiriwa.
8 Pia mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa, walimwandikia Artashasta barua ifuatayo dhidi ya Yerusalemu:
9 “Kutoka kwa mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa pamoja na wenzetu, na mahakimu, maofisa wote ambao hapo awali walitoka Ereki, Babuloni na Susa katika nchi ya Elamu,