11 Ifuatayo ni barua ambayo Artashasta alimpa Ezra, kuhani na mwandishi, na mwenye ujuzi katika amri na masharti ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa watu wa Israeli.
12 “Kutoka kwa Artashasta, mfalme wa wafalme, kwa Ezra, kuhani na mtu mwenye ujuzi katika sheria ya Mungu wa mbinguni; Wasalaam!”
13 “Ninaamuru kwamba katika utawala wangu, Mwisraeli yeyote, au kuhani wao, au Mlawi, akitaka kurudi Yerusalemu kwa hiari yake, anaweza kwenda pamoja nawe.
14 “Mimi pamoja na washauri wangu saba, tunakutuma uende ufanye uchunguzi huko Yuda na Yerusalemu kuona kama sheria ya Mungu wako ambayo umekabidhiwa inafuatwa kikamilifu.
15 Utachukua fedha na dhahabu ambayo mimi na washauri wangu tumemtolea kwa hiari Mungu wa Israeli ambaye hekalu lake limo mjini Yerusalemu.
16 Utachukua pia fedha na dhahabu yote utakayokusanya katika mkoa wote wa Babuloni, pamoja na matoleo ya hiari waliyotoa Waisraeli na makuhani wao kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu.
17 Fedha hiyo utaitumia kwa uangalifu sana kununua mafahali, kondoo dume, wanakondoo na tambiko ya nafaka na divai, na kuvitoa madhabahuni katika nyumba ya Mungu wenu iliyoko Yerusalemu.