1 Mimi nitasimama mahali pa kuchungulia,na kukaa juu mnarani;nitakaa macho nione ataniambia nini,atajibu nini kuhusu lalamiko langu.”
2 Kisha, Mwenyezi-Mungu akanijibu hivi:“Yaandike maono haya;yaandike wazi juu ya vibao,anayepitia hapo apate kuyasoma.
3 Maono haya yanangoja wakati wa kufaa;ni maono ya ukweli juu ya mwisho.Kama yaonekana kuchelewa, uyasubiri;hakika yatafika, wala hayatachelewa.
4 Andika:‘Waangalie wenye kiburi, hao wataangamia;lakini waadilifu wataishi kwa kumwamini Mungu.’”
5 Zaidi ya hayo, divai hupotosha;mtu mwenye kiburi hatadumu.Yuko tayari kuwameza wengine kama Kuzimu;kama vile kifo, hatosheki na kitu.Hujikusanyia mataifa yote,na watu wote kama mali yake.
6 Kila mtu atamdhihaki mtu wa namna hiyona kumtungia misemo ya dhihaka:“Ole wako unayejirundikia visivyo vyako,na kuchukua rehani mali za watu lakini hulipi!Utaendelea kufanya hivyo hadi lini?
7 Siku moja wadeni wako watainuka ghafla,wale wanaokutetemesha wataamka.Ndipo utakuwa mateka wao.
8 Wewe umeyapora mataifa mengi,lakini wote wanaosalimika watakupora wewe,kwa mauaji na dhuluma uliyoitendea dunia,naam, uliyoifanyia miji na wakazi wake wote.
9 “Ole wako unayejitajirisha kwa hasara ya mwingine,ujengaye nyumba yako juu milimaniukidhani kuwa salama mbali na madhara.
10 Lakini kwa mipango yako umeiaibisha jamaa yako.Kwa kuyaangamiza mataifa mengi,umeyaangamiza maisha yako mwenyewe.
11 Ndiyo maana hata mawe yatalalamika ukutani,na boriti za nyumba zitayaunga mkono.
12 “Ole wako unayejenga mji kwa mauajiunayesimika jiji kwa maovu!
13 Mwenyezi-Mungu wa majeshi husababishajuhudi za watu zipotelee motoni,na mataifa yajishughulishe bure.
14 Utukufu wa Mwenyezi-Mungu utaenea pote duniani,kama vile maji yaeneavyo baharini.
15 Ole wako unayewalewesha jirani zako,na kutia sumu katika divai yaoili upate kuwaona wamekaa uchi.
16 Utajaa aibu badala ya heshima.Utakunywa wewe mwenyewe na kupepesuka!Mwenyezi-Mungu mwenyewe atakulevya,na aibu itaifunika heshima yako!
17 Maovu uliyoitenda Lebanoni yatakuvamia wewe;uliwaua wanyama, wanyama nao watakutisha.Yote hayo yatakupata wewe,kwa mauaji na dhuluma uliyoitendea dunia,naam, uliyoifanyia miji na wakazi wake wote.
18 “Chafaa nini kinyago alichotengeneza mtu?Sanamu ni madini yaliyoyeyushwa,ni kitu cha kueneza udanganyifu!Mtengeneza sanamu hutumaini alichotengeneza mwenyewe,kinyago ambacho hakiwezi hata kusema!
19 Ole wake mtu aliambiaye gogo: ‘Amka!’Au jiwe bubu ‘Inuka!’Je, sanamu yaweza kumfundisha mtu?Tazama imepakwa dhahabu na fedha,lakini haina uhai wowote.”
20 Lakini Mwenyezi-Mungu yumo katika hekalu lake takatifu;dunia yote na ikae kimya mbele yake.