Habakuki 1 BHN

1 Kauli ya Mungu aliyoiona nabii Habakuki.

Lalamiko la nabii

2 “Ee Mwenyezi-Mungu, nitakulilia mpaka lini,nawe usinisikilize na kunisaidia?Kwa nini nalia: ‘Dhuluma’nawe hutuokoi?

3 Kwa nini wanifanya nishuhudie mabaya na taabu?Uharibifu na ukatili vinanizunguka,ugomvi na mashindano yanazuka.

4 Hivyo sheria haina nguvu,wala haki haitekelezwi.Waovu wanawazunguka waadilifu,hivyo hukumu hutolewa ikiwa imepotoshwa.”

Jibu la Mungu

5 Mungu akasema:“Yaangalie mataifa, uone!Utastaajabu na kushangaa.Maana ninatenda kitu ukiwa bado unaishi,kitu ambacho ungeambiwa hungesadiki.

6 Maana ninawachochea Wakaldayo,taifa lile kali na lenye hamaki!Taifa lipitalo katika nchi yote,ili kunyakua makao ya watu wengine.

7 Wao ni watu wa kuchukiza na kutisha;wao hujiamulia wenyewe nini haki na adhama.

8 “Farasi wao ni wepesi kuliko chui;wakali kuliko mbwamwitu wenye njaa.Wapandafarasi wao wanatoka mbali,wanaruka kasi kama tai arukiavyo mawindo.

9 “Wote wanakuja kufanya ukatili;kwa nyuso kakamavu wanasonga mbele,wanakusanya mateka wengi kama mchanga.

10 Wanawadhihaki wafalme,na kuwadharau watawala.Kila ngome kwao ni mzaha,wanairundikia udongo na kuiteka.

11 Kisha wanasonga mbele kama upepo,wafanya makosa na kuwa na hatia,maana, nguvu zao ndizo mungu wao!”

Habakuki analalamika tena

12 “Je, wewe si ndiwe Mwenyezi-Mungu,tangu kale na kale?Wewe ndiwe Mungu wangu, Mtakatifu wangu, usiyekufaEe Mwenyezi-Mungu, umewateua Wakaldayo watuhukumu;Ewe Mwamba, umewaimarisha ili watuadhibu!

13 Wewe ni mtakatifu kabisa, huwezi kutazama uovu,huwezi kustahimili kamwe kuona mabaya.Mbona basi wawaona wafanya maovu na kunyamaza,kwa nini unanyamaza waovu wanapowamalizawale watu walio waadilifu kuliko wao?

14 “Umewafanya watu kama samaki baharini,kama viumbe vitambaavyo visivyo na kiongozi!

15 Wakaldayo huwavua watu kwa ndoana,huwavutia nje kwa wavu wao,huwakusanya wote katika jarife lao,kisha hufurahi na kushangilia.

16 Kwa hiyo, wanazitambikia nyavu zao,na kuzifukizia ubani;maana kwa hizo huweza kuishi kwa anasa,na kula chakula cha fahari.

17 “Je, hawataacha kamwe kuvuta upinde wao?Je, wataendelea tu kuwanasa watu,na kuyaangamiza mataifa bila huruma?

Sura

1 2 3