35 ‘Hakuna hata mmoja wenu katika kizazi hiki kiovu atakayeingia katika nchi ile nzuri niliyoahidi kuwapa wazee wenu.
36 Kalebu mwana wa Yefune, ndiye tu atakayeiona; nami nitampatia nchi hiyo aliyoikanyaga iwe yake yeye na wazawa wake kwa kuwa amekuwa mwaminifu kabisa kwangu.’
37 Mwenyezi-Mungu alinikasirikia mimi pia kwa sababu yenu, akasema, ‘Hata wewe Mose hutaingia katika nchi hiyo.
38 Lakini msaidizi wako Yoshua mwana wa Nuni, ataingia humo. Basi, mtie moyo kwani yeye atawaongoza watu wa Israeli waimiliki nchi hiyo’.
39 Kisha Mwenyezi-Mungu akatuambia sisi sote, ‘Hao watoto wenu mnaoogopa kwamba watakuwa nyara za adui zenu, naam hao walio wadogo ambao hawajui bado kupambanua kati ya mema na mabaya, hao ndio watakaoingia huko, nami nitawapa wao nchi hiyo iwe yao.
40 Lakini nyinyi, geukeni na kurudi jangwani kuelekea Bahari ya Shamu.’
41 “Kisha mkanijibu, ‘Sisi tumemtendea dhambi Mwenyezi-Mungu, lakini sasa tutakwenda na kupigana kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru’. Hivyo, kila mmoja wenu akajitayarisha kupigana vita; maana mlifikiri kwamba lingekuwa jambo rahisi kuivamia nchi hiyo ya milima.