22 Mtaila nyama hiyo kama aliwavyo paa au kulungu. Mtu yeyote anaweza kula, aliye safi na asiye safi.
23 Ila hakikisheni kwamba hamli damu, maana damu ni uhai; hivyo basi, msile uhai pamoja na nyama.
24 Msile damu hiyo, bali imwageni chini kama maji.
25 Msile damu, nanyi mtafanikiwa pamoja na wazawa wenu, maana mtakuwa mnatenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu.
26 Vitu vitakatifu mtakavyotoa na sadaka zenu za nadhiri, mtavichukua na kuvipeleka mahali Mwenyezi-Mungu atakapochagua.
27 Hapo, mtatoa sadaka za kuteketezwa, nyama na damu, kwenye madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; damu ya mnyama mtainyunyiza kwenye madhabahu yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, lakini mnaruhusiwa kula nyama.
28 Jihadharini kutii maneno haya niliyowaamuru, ili mpate kufanikiwa nyinyi pamoja na wazawa wenu baada yenu milele, maana mtakuwa mnatenda yaliyo mema na yaliyo sawa mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.