8 Badala yake, fumbueni mikono yenu na kumkopesha kwa hiari kiasi cha kutosha mahitaji yake.
9 Angalieni wazo ovu lisiwaingie mioyoni mwenu, mkasema: ‘Mwaka wa saba, mwaka wa kusamehe wadeni, uko karibu’; mkamfikiria ndugu yenu maskini kwa ukali na kukataa kumpa chochote; yeye aweza kumlilia Mwenyezi-Mungu dhidi yenu na hiyo ikawa dhambi kwenu.
10 Mpeni ndugu maskini kwa ukarimu bila kunungunika; maana kwa ajili ya hayo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki katika kazi zenu zote na katika kila mfanyalo.
11 Maana maskini hawatakosekana nchini; hivyo nawaamuru, muwe wakarimu kwa ndugu zenu wahitaji na maskini nchini mwenu.
12 “Kama nduguyo Mwebrania, mwanamume au mwanamke, akiuzwa kwako, atakutumikia kwa miaka sita, lakini katika mwaka wa saba, utamwacha huru.
13 Nawe utakapomwacha huru, usimwache aende mikono mitupu.
14 Mpe kwa ukarimu kile ambacho Mwenyezi-Mungu amekubariki: Kondoo, nafaka na divai.