13 Muwe wakamilifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
14 “Mataifa haya ambayo mtaimiliki nchi yao hufuata maongozi ya waaguzi na wapiga ramli; lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu hawaruhusu nyinyi kufanya hivyo.
15 “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawateulieni nabii aliye kama mimi kutoka miongoni mwenu, nanyi mtamsikiliza huyo.
16 Hicho ndicho mlichomwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kule Horebu, siku ile mlipokusanyika na kusema, ‘Tusisikie tena sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wala tusiuone tena moto huu mkubwa, tusije tukafa!’
17 Naye Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Wamesema ukweli.
18 Nitawateulia miongoni mwa ndugu zao wenyewe nabii kama wewe; nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.
19 Yeyote ambaye hatasikia maneno atakayosema nabii huyo kwa jina langu, mimi mwenyewe nitamwadhibu.