7 Lakini kama huyo ndugu wa marehemu hamtaki huyo mwanamke mjane, basi, mwanamke huyo atakwenda mbele ya wazee wa mji na kusema, ‘Kaka wa mume wangu marehemu anakataa kuendeleza jina la kaka yake marehemu katika Israeli; hapendi kunitimizia jukumu lake la kaka wa mume wangu marehemu.’
8 Kisha wazee wa mji watamwita huyo mwanamume kuongea naye. Kama bado atasisitiza kwamba hataki kumwoa,
9 huyo mwanamke mjane atamwendea mbele ya hao wazee wa mji, atamvua kiatu chake kimoja na kumtemea mate usoni na kumwambia, ‘Hivi ndivyo anavyopaswa kutendewa mtu anayekataa kuidumisha nyumba ya kaka yake.’
10 Na jina la nyumba yake katika Israeli litakuwa: ‘Nyumba ya mtu aliyevuliwa kiatu.’”
11 “Wanaume wawili wakipigana na mke wa mmoja wao akamsaidia mumewe kwa kumkamata sehemu za siri yule anayepigana na mumewe,
12 mtaukata mkono wa kulia wa huyo mwanamke; msimhurumie.
13 “Msiwe na vipimo vya kupimia vya namna mbili: Kimoja kizito na kingine chepesi. Msitumie mizani za udanganyifu.