2 Kama mkitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mtapewa baraka zifuatazo;
3 “Miji yenu itabarikiwa na mashamba yenu.
4 “Mtabarikiwa mpate wazawa wengi, mavuno mengi, ng'ombe na kondoo wengi.
5 “Vikapu vyenu vya nafaka vitabarikiwa na vyombo vyenu vya kukandia.
6 Mtabarikiwa mnaporudi nyumbani na mnapotoka nje.
7 Maadui zenu wakiwashambulia, Bwana atawapeni ushindi juu yao. Wakija kuwashambulia kwa njia moja watawakimbieni kwa njia saba.
8 Baraka za Mwenyezi-Mungu zitakuwa katika ghala zenu za nafaka na katika shughuli zenu zote. Atawabariki katika nchi ambayo anawapeni.