39 Mtapanda mizabibu na kuitunza, lakini hamtavuna mizabibu hiyo wala kunywa divai yake, maana wadudu wataila.
40 Mtakuwa na mizeituni mahali pote nchini mwenu, lakini hamtakuwa na mafuta ya kujipaka; kwa sababu zeituni hizo zitapukutika.
41 Mtazaa watoto wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa wenu, watachukuliwa uhamishoni.
42 Matunda yenu yote na mazao yenu mashambani vitamilikiwa na nzige.
43 “Wageni waishio katika nchi yenu watazidi kupata nguvu huku nyinyi mkizidi kufifia zaidi na zaidi.
44 Wao watawakopesha nyinyi, lakini nyinyi hamtakuwa na uwezo wa kuwakopesha. Wao watakuwa wa kwanza kwa nguvu nanyi mtakuwa wa mwisho.
45 “Hayo yote yatawapateni nyinyi na kuwaandama mpaka muangamizwe kwa kuwa hamkutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kuhusu kushika amri zake na masharti aliyowapa.