12 Usingizi wa kibarua ni mtamu, awe ameshiba au amekula kidogo tu. Lakini usingizi wa tajiri ni wa wasiwasi daima, maana ziada ya mali yake humsumbua usiku kucha.
13 Tena, nimeona jambo moja ovu sana duniani: Mtu alijirundikia mali ikawa hatari kwake.
14 Kwa bahati mbaya, mali hiyo iliharibiwa katika matumizi mabaya, mwisho, mtu huyo hakuwa na chochote mkononi na alikuwa na mwana.
15 Kama vile binadamu alivyokuja duniani uchi toka tumboni mwa mama yake, ndivyo atakavyorudi uchi huko alikotoka. Hataweza kuchukua hata sehemu ndogo ya mapato ya kazi yake.
16 Hili nalo ni jambo baya sana. Atarudi kama alivyokuja. Amejisumbua kufukuza upepo, akatoka jasho bure.
17 Aliishi maisha yake yote katika giza na huzuni; katika mahangaiko, magonjwa na hasira.
18 Basi, haya ndiyo niliyogundua: Jambo zuri na la kufaa kwa binadamu ni kula, kunywa na kufurahia matunda ya jasho analotoa katika kazi anayoifanya hapa duniani, siku hizo chache za maisha aliyojaliwa na Mungu, maana hivyo ndivyo alivyopangiwa.