4 Mtoto mfu hafaidiki chochote kwa kuzaliwa; yeye hutokomea gizani, akasahaulika.
5 Zaidi ya hayo, mtoto wa namna hiyo hakupata kuuona mwanga wa jua wala kutambua chochote. Hata hivyo, huyo mtoto angalau hupata pumziko ambapo yule mtu hapati.
6 Ingawa mtu huyo ataishi miaka elfu mbili, lakini hafurahii maisha, basi ni kama huyo mtoto wote wawili huenda mahali pamoja.
7 Kazi yote ya mtu ni kwa ajili ya kupata chakula, lakini tamaa yake ya kula haitoshelezwi kamwe.
8 Je, mtu mwenye hekima anayo nafuu zaidi kuliko mpumbavu? Na mtu maskini hupata faida gani akijua namna ya kuyakabili maisha?
9 Hayo nayo ni bure kabisa; ni sawa na kufukuza upepo. Afadhali kuridhika na ulicho nacho kuliko kuhangaika kwa kutamani kitu kingine.
10 Kila kitu kinachotukia kilikwisha pangwa hapo awali; hali ya binadamu inajulikana, na tunajua kwamba mnyonge hawezi kubishana na mtu mwenye nguvu zaidi.