2 Tii amri ya mfalme, kwa sababu ya kiapo chako kitakatifu.
3 Usifanye haraka kuondoka mbele yake; wala usiwe na kiburi juu ya jambo baya, maana mfalme hufanya apendavyo.
4 Amri ya mfalme ni kauli ya mwisho; nani athubutuye kumwuliza, “Unafanya nini?”
5 Anayetii amri hatapata madhara, na mwenye hekima atajua kuna wakati na njia.
6 Naam, kila kitu kina wakati wake na njia yake, ingawa binadamu anakabiliwa na tatizo kubwa:
7 Hajui ni nini kitakachotukia baadaye, kwani nani awezaye kumjulisha yatakayotukia baadaye?
8 Hakuna mtu aliye na uwezo wa kushikilia roho yake asife; hakuna mtu aliye na uwezo juu ya siku ya kufa. Wakati wa vita hakuna kuponyoka, na uovu hauwezi kumwokoa mwovu.