8 Basi hao wapelelezi walirudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, nao wakawauliza, “Mmetuletea taarifa gani?”
9 Wao wakasema, “Inukeni twende na kuishambulia nchi hiyo. Tumeiona nchi hiyo, na kweli ni nchi yenye rutuba. Je, mtakaa hapa tu bila kufanya kitu? Msikawie kwenda kuimiliki nchi hiyo.
10 Mtakapofika huko mtakuta watu wasio na wasiwasi wowote. Nchi hiyo ni kubwa, haikupungukiwa chochote na Mungu ameitia mikononi mwetu.”
11 Basi, watu 600 wa kabila la Dani wakiwa na silaha zao za vita wakaondoka kutoka Sora na Eshtaoli
12 wakaenda kupiga kambi yao huko Kiriath-yearimu katika nchi ya Yuda. Ndiyo maana mahali hapo, upande wa magharibi wa Kiriath-yearimu pameitwa Mahane-dani mpaka leo.
13 Kutoka huko wakaelekea nchi ya milima ya Efraimu, wakafika nyumbani kwa Mika.
14 Watu wale watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mnajua kwamba katika nyumba mojawapo ya hizi kuna kizibao, kinyago na sanamu ya kusubu? Basi, fikirini namna ya kufanya.”