1 Mwenyezi-Mungu aliyaacha nchini mataifa yafuatayo ili kuwajaribu Waisraeli ambao walikuwa hawajapigana vita katika nchi ya Kanaani
2 (alifanya hivyo ili awape watu wa vizazi hivyo ujuzi wa kupigana kwani hawakuwa wameona vita):
3 Wakuu watano wa Wafilisti, Wakanaani wote, Wasidoni na Wahivi waliohamia katika milima ya Lebanoni kutoka mlima Baal-hermoni mpaka kufikia Hamathi.
4 Mwenyezi-Mungu alikusudia kuwatumia hao ili awajaribu Waisraeli, aone kama watatii amri zake alizowaamuru wazee wao kwa njia ya Mose.
5 Basi, Waisraeli waliishi pamoja na Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.
6 Wakaoa binti zao na kuoza binti zao kwa vijana wa mataifa hayo na kuiabudu miungu yao.
7 Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; wakamsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakaabudu Mabaali na Maashera.
8 Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia, nao wakamtumikia kwa muda wa miaka minane.
9 Waisraeli wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawapelekea mtu wa kuwakomboa yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu.
10 Basi, roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Othnieli, naye akawa mwamuzi wa Waisraeli. Othnieli alikwenda vitani naye Mwenyezi-Mungu akamtia Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia mikononi mwake.
11 Hivyo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini. Kisha Othnieli mwana wa Kenazi, akafariki.
12 Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akampa nguvu mfalme Egloni wa Moabu awashambulie Waisraeli, kwa sababu walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu.
13 Egloni akawakusanya Waamoni na Waamaleki, akaenda kupigana na Waisraeli, akawashinda. Akauteka Mji wa Mitende yaani Yeriko.
14 Waisraeli wakamtumikia Egloni mfalme wa Moabu, kwa muda wa miaka kumi na minane.
15 Lakini Waisraeli walipomlilia Mwenyezi-Mungu, yeye aliwapelekea mtu wa kuwakomboa, yaani Ehudi mwana wa Gera, mwenye mkono wa shoto, wa kabila la Benyamini.Waisraeli walimtuma apeleke zawadi zao kwa Egloni mfalme wa Moabu.
16 Ehudi akajitengenezea upanga wenye makali kuwili; urefu wake sentimita hamsini. Akaufunga kiunoni mwake upande wa kulia ndani ya mavazi yake.
17 Kisha akampelekea Egloni zile zawadi. Egloni alikuwa mtu mnene sana.
18 Ehudi alipomaliza kutoa zawadi, akawaambia watu waliobeba zawadi, waondoke.
19 Lakini yeye alipofika kwenye sanamu za mawe yaliyochongwa karibu na Gilgali, alimrudia Egloni akasema, “Nina ujumbe wa siri kwako, ee mfalme.” Mfalme akawaamuru watumishi wakae kimya, nao wakatoka nje.
20 Naye Ehudi akamkaribia pale alipokaa katika chumba chake chenye baridi barazani, akamwambia “Nina ujumbe wako kutoka kwa Mungu.” Mfalme akainuka kitini mwake na kusimama.
21 Ehudi akauchomoa upanga wake kwa mkono wake wa kushoto kutoka paja lake la kulia, akamchoma nao tumboni mwake.
22 Upanga ukaingia ndani pamoja na mpini wake, mafuta yakaufunika upanga huo kwani Ehudi hakuutoa tena; ukawa umetokea kwa nyuma.
23 Kisha, Ehudi akatoka nje barazani baada ya kuifunga milango ya chumba hicho kwa ufunguo.
24 Ehudi alipoondoka, watumishi wa mfalme wakarudi. Walipoona milango yote ya chumba imefungwa, walifikiri amekwenda kujisaidia chooni humo ndani ya nyumba.
25 Wakangojea mpaka wakaanza kuwa na wasiwasi. Walipoona hafungui, wakachukua ufunguo na kufungua mlango. Wakamwona mfalme wao sakafuni, naye amekufa.
26 Walipokuwa wanangoja, Ehudi alitoroka akipitia kwenye sanamu za mawe, akaenda Seira.
27 Alipofika huko alipiga tarumbeta katika nchi ya milima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka huko milimani naye akawatangulia.
28 Akawaambia, “Mnifuate, maana Mwenyezi-Mungu amewatia adui zenu Wamoabu mikononi mwenu.” Wakamfuata mpaka kivuko cha Yordani na kukiteka toka mikononi mwa Wamoabu, wakazuia mtu yeyote kupita.
29 Siku hiyo, wakawaua Wamoabu wapatao 10,000; watu wote wenye afya na nguvu, wala hakuna hata mmoja aliyenusurika.
30 Siku hiyo Waisraeli wakawashinda Wamoabu. Nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka themanini.
31 Baada ya Ehudi mwana wa Anati, Shamgari alishika nafasi yake. Yeye aliwaua Wafilisti 600 kwa fimbo ya kuchungia ng'ombe. Naye pia aliwakomboa Waisraeli.