1 Wakati huo ambapo hapakuwepo na mfalme katika Israeli, kulikuwa na Mlawi fulani aliyeishi kama mgeni mbali katika eneo la milima ya Efraimu. Mtu huyo alichukua suria kutoka Bethlehemu nchini Yuda.
2 Lakini suria huyo akamkasirikia; huyo Mlawi, akamwacha na kurudi nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu, akakaa kwa muda wa miezi minne.
3 Siku moja, mumewe alikwenda kumtafuta; alikusudia kuongea naye vizuri na kumrudisha nyumbani kwake. Basi huyo mwanamume alikwenda pamoja na mtumishi wake na punda wawili. Basi yule mwanamke akampeleka ndani kwa baba yake, naye baba mkwe wake alipomwona akampokea kwa furaha.
4 Baba mkwe wake akamkaribisha, naye akakaa huko kwa muda wa siku tatu; huyo Mlawi na mtumishi wake wakala, wakanywa na kulala huko.
5 Siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, wakajitayarisha kuondoka; lakini baba wa yule mwanamke akamwambia, “Kwanza kula chakula kidogo upate nguvu, kisha uondoke.”
6 Basi hao watu wawili wakakaa, wakala na kunywa pamoja. Kisha baba mkwe wake akamwambia, “Tafadhali ulale hapa usiku huu na kufurahi.”