1 Mwenyezi-Mungu aliyaacha nchini mataifa yafuatayo ili kuwajaribu Waisraeli ambao walikuwa hawajapigana vita katika nchi ya Kanaani
2 (alifanya hivyo ili awape watu wa vizazi hivyo ujuzi wa kupigana kwani hawakuwa wameona vita):
3 Wakuu watano wa Wafilisti, Wakanaani wote, Wasidoni na Wahivi waliohamia katika milima ya Lebanoni kutoka mlima Baal-hermoni mpaka kufikia Hamathi.
4 Mwenyezi-Mungu alikusudia kuwatumia hao ili awajaribu Waisraeli, aone kama watatii amri zake alizowaamuru wazee wao kwa njia ya Mose.
5 Basi, Waisraeli waliishi pamoja na Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.
6 Wakaoa binti zao na kuoza binti zao kwa vijana wa mataifa hayo na kuiabudu miungu yao.
7 Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; wakamsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakaabudu Mabaali na Maashera.