1 Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli:
2 Sikilizeni kitu hiki enyi wazee;tegeni sikio wakazi wote wa Yuda!Je, jambo kama hili limewahi kutokea maishani mwenu,au nyakati za wazee wenu?
3 Wasimulieni watoto wenu jambo hili,nao wawasimulie watoto wao,na watoto wao wakisimulie kizazi kifuatacho.
4 Nzige, makundi kwa makundi, wameivamia mimea;kilichoachwa na nzige kimeliwa na tunutu,kilichoachwa na tunutu kimeliwa na parare,kilichoachwa na parare kimeliwa na matumatu.
5 Enyi walevi, levukeni na kulia;pigeni yowe, enyi walevi wa divai;zabibu zote za kutengeneza divai mpya zimeharibiwa.
6 Jeshi la nzige limeivamia nchi yetu;lina nguvu na ni kubwa ajabu;meno yake ni kama ya simba,na magego yake ni kama ya simba jike.