1 Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli:
2 Sikilizeni kitu hiki enyi wazee;tegeni sikio wakazi wote wa Yuda!Je, jambo kama hili limewahi kutokea maishani mwenu,au nyakati za wazee wenu?
3 Wasimulieni watoto wenu jambo hili,nao wawasimulie watoto wao,na watoto wao wakisimulie kizazi kifuatacho.
4 Nzige, makundi kwa makundi, wameivamia mimea;kilichoachwa na nzige kimeliwa na tunutu,kilichoachwa na tunutu kimeliwa na parare,kilichoachwa na parare kimeliwa na matumatu.
5 Enyi walevi, levukeni na kulia;pigeni yowe, enyi walevi wa divai;zabibu zote za kutengeneza divai mpya zimeharibiwa.
6 Jeshi la nzige limeivamia nchi yetu;lina nguvu na ni kubwa ajabu;meno yake ni kama ya simba,na magego yake ni kama ya simba jike.
7 Limeiharibu mizabibu yetu,na kuitafuna mitini yetu.Limeyabambua magamba yake na kuyatupa chini,na matawi yake yameachwa meupe.
8 Lieni kama msichana aliyevaa vazi la guniaakiombolezea kifo cha mchumba wake.
9 Sadaka za nafaka na kinywaji zimetoweka nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu.Makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu, wanaomboleza.
10 Mashamba yamebaki matupu;nchi inaomboleza,maana nafaka imeharibiwa,divai imetoweka,mafuta yamekosekana.
11 Ombolezeni enyi wakulima;pigeni yowe enyi watunza mizabibu.Ngano na shayiri zimeharibika,mavuno yote shambani yameangamia.
12 Mizabibu imenyauka;mitini imedhoofika;mikomamanga, mitende na mitofaa imekauka,naam miti yote shambani imekauka.Furaha imetoweka miongoni mwa watu.
13 Enyi makuhani, jivikeni magunia kuomboleza,lieni enyi wahudumu wa madhabahu.Ingieni hekaluni mkaomboleze usiku kucha!Sadaka za nafaka na kinywaji zimetoweka nyumbani kwa Mungu.
14 Toeni amri watu wafunge;itisheni mkutano wa kidini.Kusanyeni wazee na wakazi wote wa nchi,nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,na humo mkamlilie Mwenyezi-Mungu.
15 Ole wetu kwa ile siku ya Mwenyezi-Mungu,siku hiyo ya Mwenyezi-Mungu inakaribia;inakuja pamoja na maangamizi,kutoka kwa Mungu Mkuu.
16 Mazao yetu yameharibiwa huku tunatazama.Furaha na kicheko vimetoweka nyumbani kwa Mungu wetu.
17 Mbegu zinaoza udongoni;ghala za nafaka ni ukiwa mtupu,ghala zimeharibika,kwa kukosa nafaka ya kuhifadhi.
18 Tazama wanyama wanavyolia kwa huzuni!Makundi ya ng'ombe yanahangaika,kwa sababu yamekosa malisho;hata makundi ya kondoo yanateseka.
19 Ninakulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu,moto umemaliza malisho nyikani,miali ya moto imeteketeza miti mashambani.
20 Hata wanyama wa porini wanakulilia wewe,maana, vijito vya maji vimekauka,moto umemaliza malisho nyikani.