1 Siku moja, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yona, mwana wa Amitai:
2 “Ondoka uende Ninewi, ule mji mkuu, ukaukemee, maana nimeona uovu wake ni mkubwa mno.”
3 Basi, Yona akaanza safari, lakini akashika njia ya kwenda Tarshishi ili kumkwepa Mwenyezi-Mungu. Akaenda hadi mjini Yopa ambapo alikuta meli moja iko tayari kwenda Tarshishi. Alilipa nauli, akapanda meli, akasafiri na mabaharia hao kwenda Tarshishi ili kumkwepa Mwenyezi-Mungu.
4 Lakini Mwenyezi-Mungu akavumisha upepo mkali baharini, ikatokea dhoruba kali, meli ikawa karibu kabisa kuvunjika.
5 Mabaharia wakajawa na hofu, kila mmoja akaanza kumlilia mungu wake; wakatupa baharini shehena ya meli ili kupunguza uzito wake. Wakati huo, Yona alikuwa ameteremkia sehemu ya ndani ya meli, akawa amelala usingizi mzito.