1 Neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yona mara ya pili:
2 “Nenda Ninewi, ule mji mkuu, ukawatangazie watu ujumbe niliokupa.”
3 Basi, Yona akaondoka, akaenda Ninewi kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza.Mji wa Ninewi ulikuwa mkubwa sana. Upana wake ulikuwa mwendo wa siku tatu.
4 Alipowasili, Yona aliingia mjini, na baada ya kutembea mwendo wa siku nzima, akaanza kutangaza: “Bado siku arubaini tu na mji huu wa Ninewi utaangamizwa!”
5 Basi, watu wa Ninewi wakauamini ujumbe wa Mungu, wakatangaza mfungo, na kwamba kila mmoja wao, mkubwa kwa mdogo, avae vazi la gunia kama ishara ya kutubu.
6 Habari hizi zikamfikia mfalme wa Ninewi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake rasmi, akajivika vazi la gunia na kuketi katika majivu.
7 Kisha mfalme akawatangazia wakazi wa Ninewi: “Mimi mfalme, pamoja na wakuu wangu, natoa amri hii: Pasiwe na binadamu yeyote, ng'ombe au mnyama yeyote wa kufugwa, atakayeonja kitu chochote. Ni mwiko kwa mtu yeyote au mnyama kula au kunywa.
8 Watu wote na wanyama wavae mavazi ya gunia. Kila mtu na amwombe Mungu na kumsihi kwa moyo. Naam, kila mmoja na aache uovu na ukatili wake.
9 Huenda Mungu akabadili nia yake, akaacha kutukasirikia, tusije tukaangamia!”
10 Mungu alipoona walivyofanya, na jinsi walivyouacha uovu wao, akabadili nia yake, akaacha kuwatenda kama alivyokuwa amekusudia.