1 Basi, Yona, akiwa tumboni mwa samaki huyo, akawa akimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake,
2 akisema:“Kwa sababu ya taabu yangu,nilikuomba, ee Mwenyezi-Mungu,nawe ukanisikiliza;toka chini kuzimu, nilikulilia,nawe ukasikiliza kilio changu.
3 Ulinitupa katika kilindi, katikati ya bahari,gharika ikanizunguka,mawimbi na gharika vikapita juu yangu.
4 Nilidhani kwamba nimetengwa nisiwe mbele yako;nisiweze kuliona tena hekalu lako takatifu.
5 Maji yalinizunguka na kunisonga;kilindi kilinifikia kila upande,majani ya baharini yakanifunika kichwa.
6 Niliteremka hadi kwenye misingi ya milima,katika nchi ambayo milango yake imefungwa milele.Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu,umenipandisha hai kutoka humo shimoni.
7 Roho yangu ilipoanza kunitoka,nilikukumbuka, ee Mwenyezi-Mungu,sala yangu ikakufikia,katika hekalu lako takatifu.