5 Kisha wafalme hao watano wa Waamori: Mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni, wakaunganisha majeshi yao, wakaenda nayo mpaka Gibeoni; wakapiga kambi kuuzingira mji huo, wakaushambulia.
6 Wagibeoni wakapeleka ujumbe kwa Yoshua huko kambini Gilgali, wakamwambia, “Tafadhali, usitutupe sisi watumishi wako; njoo upesi utusaidie na kutuokoa kwa maana wafalme wote wa Waamori kutoka nchi ya milimani wamekuja kutushambulia.”
7 Basi, Yoshua pamoja na jeshi lake lote na mashujaa wakaondoka Gilgali.
8 Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope hata kidogo maana nimewatia mikononi mwako, wala hakuna hata mmoja atakayeweza kukukabili.”
9 Baada ya kutembea kutoka Gilgali usiku kucha, Yoshua akawatokea ghafla.
10 Naye Mwenyezi-Mungu akawatia hofu kuu mbele ya Waisraeli ambao waliwaua watu wengi huko Gibeoni wakiwakimbiza kwenye njia ya mteremko wa Beth-horoni mpaka Azeka na Makeda ambako pia waliwaua watu wengi sana.
11 Walipokuwa wakiwakimbia Waisraeli kwenye mteremko wa Beth-horoni, Mwenyezi-Mungu akawanyeshea mvua ya mawe makubwa kutoka mbinguni wakiwa njiani mpaka Azeka hata waliouawa kwa mawe hayo wakawa wengi kuliko waliouawa kwa silaha za Waisraeli.