5 Basi, Waisraeli wakaigawanya nchi kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
6 Siku moja watu wa kabila la Yuda walimwendea Yoshua huko Gilgali. Kalebu mwana wa Yefune, ambaye alikuwa Mkenizi, akamwambia Yoshua, “Bila shaka unakumbuka jinsi Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose, mtu wa Mungu, juu yangu na wewe tulipokuwa Kadesh-barnea:
7 Nilipokuwa na umri wa miaka arubaini, Mose mtumishi wa Mungu, alinituma kutoka Kadesh-barnea, kwenda kuipeleleza nchi. Niliporudi nilimletea habari za mambo ya huko kadiri nilivyoamini moyoni mwangu,
8 hali wale wenzangu waliokwenda pamoja nami waliwavunja watu moyo, lakini mimi nilimfuata Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kwa uaminifu.
9 Siku hiyo Mose aliniapia, ‘Hakika sehemu ya nchi ile ambayo ulipita itakuwa yako wewe na wazawa wako milele. Kwa sababu ya uaminifu wako kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako’.
10 Lakini sasa tazama! Ni muda wa miaka arubaini na mitano tangu Mwenyezi-Mungu alipoongea na Mose, wakati Waisraeli walipokuwa wanapitia jangwani. Tangu wakati huo Mwenyezi-Mungu, kama alivyoahidi, amenihifadhi hai mpaka leo, na sasa mimi nina umri wa miaka themanini na mitano.
11 Lakini bado nina nguvu kama nilivyokuwa wakati ule Mose aliponituma. Hata sasa nina nguvu za kuweza kupigana vita au kufanya kazi nyingine yoyote.