10 Maana tumesikia jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu mlipotoka nchi ya Misri, na jinsi mlivyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ngambo ya mto Yordani, yaani Sihoni na Ogu, ambao mliwaangamiza kabisa.
11 Mara tu tuliposikia mambo hayo, tulikufa moyo kabisa kwa sababu yenu, tukaishiwa nguvu kabisa. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu juu mbinguni na chini duniani!
12 Kwa hiyo basi, tafadhali mniapie kwa jina la Mwenyezi-Mungu kwamba mtanitendea kwa wema mimi na jamaa yangu kama vile mimi nilivyowatendeeni kwa wema, na mnipe uthibitisho kamili.
13 Ahidini kwamba mtamsalimisha baba yangu na mama yangu, kaka zangu na dada zangu, na jamaa yao yote; hamtakubali tuuawe!”
14 Wale watu wakamjibu, “Uhai wenu ni uhai wetu! Kama hamtaifichua siri yetu, Mwenyezi-Mungu atakapotupa nchi hii, tutakutendea kwa wema na uaminifu.”
15 Basi, Rahabu akawashusha hao watu kwa kamba kupitia dirishani, kwa kuwa nyumba yake ilikuwa imejengwa ikiambatana na ukuta wa mji wa Yeriko.
16 Akawaambia: “Nendeni mlimani mkajifiche huko ili wanaowafuatia wasiwakute. Kaeni huko kwa muda wa siku tatu, mpaka wanaowafuatia watakapokuwa wamerudi mjini, kisha mwende zenu.”