19 Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga.
20 Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile.
21 Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; ikiwa ashona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi.
22 Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya.
23 Ikawa alipokuwa akipita mashambani siku ya sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke.
24 Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato?
25 Akawaambia, Hamkusoma popote alivyofanya Daudi, alipokuwa ana haja, na kuona njaa, yeye na wenziwe?