31 Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula.
32 Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu.
33 Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika.
34 Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35 Hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa;
36 uwaage watu hawa, ili waende zao mashambani na vijijini kandokando, wakajinunulie chakula.
37 Akajibu, akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakamwambia, Je! Twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape kula?