18 Mimi ndimi ninayejishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenipeleka ananishuhudia.
19 Basi wakamwambia, Yuko wapi Baba yako? Yesu akajibu, Mimi hamnijui, wala Baba yangu hammjui; kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba yangu.
20 Maneno hayo aliyasema alipokuwa akifundisha hekaluni, katika chumba cha hazina; wala hakuna mtu aliyemkamata, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.
21 Basi akawaambia tena, Mimi naondoka, nanyi mtanitafuta; nanyi mtakufa katika dhambi yenu; mimi niendako ninyi hamwezi kuja.
22 Basi Wayahudi wakasema, Je! Atajiua! Kwa kuwa asema, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja?
23 Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.
24 Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.