23 Tena, Mungu akamwondokeshea adui mwingine, Rezoni mwana wa Eliada, aliyemkimbia bwana wake Hadadezeri mfalme wa Soba,
24 naye akakusanya watu, akawa mkuu wa jeshi, hapo Daudi alipowaua hao watu wa Soba; wakaenda Dameski, wakakaa humo, na kumiliki huko Dameski.
25 Naye akawa adui wa Israeli siku zote za Sulemani, zaidi ya madhara yake Hadadi; naye akawachukia Israeli, akamiliki juu ya Shamu.
26 Na Yeroboamu wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumwa wake Sulemani; ambaye jina lake mamaye aliitwa Serua, mwanamke aliyefiwa na mumewe; yeye naye akainua mkono wake juu ya mfalme.
27 Na hii ndiyo sababu ya yeye kumwinulia mfalme mkono. Sulemani aliijenga Milo, akapafunga palipobomoka pa mji wa baba yake Daudi.
28 Na huyo Yeroboamu alikuwa mtu hodari, shujaa; Sulemani akaona ya kuwa kijana huyo ni mtu mwenye bidii, akamweka juu ya kazi yote ya nyumba ya Yusufu.
29 Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani.