38 Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.
39 Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye Mungu, BWANA ndiye Mungu.
40 Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko.
41 Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele.
42 Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini.
43 Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba.
44 Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie.