7 Na Obadia alipokuwa njiani, kumbe! Eliya akakutana naye. Akamtambua, akaanguka kifudifudi, akanena, Je! Ni wewe, bwana wangu Eliya?
8 Akamjibu, Ni mimi. Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.
9 Akamwambia, Nimekosa nini, hata unitie mimi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu, aniue?
10 Kama BWANA, Mungu wako, aishivyo, hakuna taifa wala ufalme ambao bwana wangu hakutuma watu wakutafute; na waliposema, Hayupo, akawaapisha ule ufalme, na taifa, ya kwamba hawakukuona.
11 Nawe sasa wasema, Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.
12 Na itakuwa, mara mimi nikiondoka kwako, roho ya BWANA atakuchukua uende nisikojua; nami nitakapokwenda kumwambia Ahabu, naye asipokuona, ataniua, lakini mimi mtumishi wako namcha BWANA tangu ujana wangu.
13 Je! Bwana wangu hakuambiwa nilivyofanya hapo Yezebeli alipowaua manabii wa BWANA? Jinsi nilivyowaficha manabii wa BWANA, watu mia, hamsini hamsini katika pango, nikawalisha chakula na kuwapa maji?