24 Basi kwa hiyo, BWANA aishivyo, aliyenithibitisha na kunikalisha katika kiti cha enzi cha Daudi baba yangu, akanifanyia nyumba, kama alivyoahidi, hakika atauawa leo hivi Adonia.
25 Mfalme Sulemani akatuma kwa mkono wa Benaya mwana wa Yehoyada: naye akampiga, hata akafa.
26 Tena, mfalme akamwambia Abiathari kuhani, Enenda Anathothi mashambani kwako; kwa kuwa wastahili kufa; ila leo sikuui, kwa sababu wewe ulichukua sanduku la Bwana mbele ya Daudi baba yangu, na kwa sababu wewe uliteswa kwa mateso yote ya baba yangu.
27 Hivyo Sulemani akamtoa Abiathari asiwe kuhani wa BWANA; ili alitimize neno la BWANA, alilonena juu ya nyumba ya Eli katika Shilo.
28 Tena, habari zikamfikia Yoabu; kwa maana Yoabu alikuwa amemfuata Adonia, ingawa hakumfuata Absalomu. Yoabu akakimbilia Hemani kwa BWANA, akazishika pembe za madhabahu.
29 Akaambiwa mfalme Sulemani ya kwamba, Yoabu amekimbilia Hemani kwa BWANA, naye, tazama, yuko madhabahuni. Ndipo Sulemani akamtuma Benaya, mwana wa Yehoyada, akisema, Enenda, umpige.
30 Basi Benaya akaja Hemani kwa BWANA, akamwambia, Mfalme asema hivi, Njoo utoke. Naye akajibu, La, sivyo; ila nitakufa papa hapa. Naye Benaya akamletea mfalme habari, akisema, Hivi ndivyo alivyonena Yoabu, na ndivyo alivyonijibu.