34 Na Ben-hadadi akamwambia, Miji ile baba yangu aliyomnyang’anya baba yako nitairudisha; nawe utajifanyia njia huko Dameski, kama baba yangu aliyoifanya huko Samaria. Ahabu akasema, Nami nitakuacha kwa mapatano haya. Akafanya mapatano naye, akamwacha.
35 Basi, mtu mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake kwa neno la BWANA, Nipige, nakusihi. Akakataa yule kumpiga.
36 Akamwambia, Kwa sababu hukuisikiliza sauti ya BWANA, angalia, mara ukitoka kwangu simba atakuua. Na mara alipotoka kwake, simba alimwona, akamwua.
37 Ndipo akaona mtu mwingine, akasema, Nipige, nakusihi. Yule mtu akampiga, hata kumpiga na kumtia jeraha.
38 Basi yule nabii akaenda akamngoja mfalme njiani, amejibadilisha kwa kilemba juu ya macho yake.
39 Ikawa mfalme alipopita, alimwita mfalme; akasema, Mtumwa wako aliingia katikati ya pigano; na tazama, mtu mmoja akanigeukia akaniletea mtu, akaniambia, Umlinde mtu huyu; akipotea kwa njia yo yote, roho yako itakuwa mahali pa roho yake, au utatoa talanta ya fedha.
40 Ikawa mtumishi wako alipokuwa akitenda haya na haya, yule akaenda zake. Mfalme wa Israeli akamwambia, Ndivyo itakavyokuwa hukumu yako; umejihukumu mwenyewe.