18 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?
19 Mikaya akasema, Sikia basi neno la BWANA; Nalimwona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto.
20 BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.
21 Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya.
22 BWANA akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.
23 Basi angalia, BWANA ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye BWANA amenena mabaya juu yako.
24 Ndipo akakaribia Zedekia, mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Roho ya BWANA alitokaje kwangu ili aseme na wewe?