33 Ikawa, wakuu wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.
34 Mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari lake, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.
35 Pigano likazidi siku ile; mfalme akategemezwa garini mwake, kinyume cha Washami, hata jioni akafa; damu ikatoka katika jeraha yake ndani ya gari.
36 Ikapigwa mbiu jeshini, jua likichwa, kusema, Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake.
37 Hivyo akafa mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria.
38 Wakaliosha gari penye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake; (basi ndipo walipooga makahaba); sawasawa na neno la BWANA alilolinena.
39 Na mambo yote ya Ahabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na nyumba ya pembe aliyoijenga, na miji yote aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?