7 Ikawa, Hiramu aliposikia maneno yake Sulemani, alifurahi sana, akasema, Na ahimidiwe BWANA leo, aliyempa Daudi mwana mwenye akili juu ya watu hawa walio wengi.
8 Hiramu akatuma watu kwa Sulemani, akasema, Nimeyasikia yale uliyoniletea; nami nitafanya kila ulitakalo katika habari ya miti ya mierezi, na miti ya miberoshi.
9 Watumishi wangu wataishusha toka Lebanoni mpaka baharini; nami nitaiendesha baharini, ikifungwa pamoja, mpaka mahali utakaponiagiza, huko nitaifungua ili wewe uichukue; ndivyo utakavyoitimiza haja yangu, ukiwapa chakula watu wa nyumbani mwangu.
10 Basi Hiramu akampa Sulemani miti ya mierezi na miti ya miberoshi kadiri alivyotaka.
11 Sulemani akampa Hiramu kori ishirini elfu za ngano, chakula cha watu wake, na kori ishirini za mafuta safi. Ndizo Sulemani alizompa Hiramu mwaka kwa mwaka.
12 BWANA akampa Sulemani hekima, kama alivyomwahidia. Ikawa amani kati yao Hiramu na Sulemani; wakafanyana maagano pamoja hao wawili.
13 Mfalme Sulemani akafanya shokoa ya Israeli wote; nayo shokoa hiyo ilikuwa ya watu thelathini elfu.