18 Hivyo akazifanya nguzo; na kulikuwa na safu mbili za kuzunguka juu ya wavu mmoja, zifunike taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; akafanya vivyo hivyo kwa taji ya pili.
19 Na taji zilizokuwa juu ya nguzo ukumbini zilikuwa za kazi ya mayungi, mikono minne.
20 Kulikuwako tena taji juu ya nguzo mbili, karibu na uvimbe uliokuwako kando ya wavu; na makomamanga yalikuwa mia mbili, safu safu pande zote juu ya taji ya pili.
21 Akazisimamisha nguzo ukumbini pa hekalu; akaisimamisha nguzo ya kuume, akaiita jina lake Yakini; akaisimamisha nguzo ya kushoto, akaiita jina lake Boazi.
22 Na juu ya nguzo kulikuwa na kazi ya mayungi; hivyo mambo ya nguzo yakatimia.
23 Tena akaifanya bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ikaviringana, na mikono mitano ilikuwa kwenda juu kwake; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa.
24 Na chini ya ukingo wake kulikuwa na maboga yaliyoizunguka, kwa mikono kumi, yakiizunguka bahari; kulikuwa na safu mbili za hayo maboga, yakafanywa kalibuni hapo bahari ilipofanywa.